Hamia kwenye habari

KOREA KUSINI

Maelezo Mafupi Kuhusu Korea Kusini

Maelezo Mafupi Kuhusu Korea Kusini

Mashahidi wa Yehova wamekuwapo Korea kwa zaidi ya miaka 100 na wameabudu kwa uhuru. Tatizo kubwa wanalokabili Mashahidi nchini Korea Kusini ni kuendelea kuteswa na serikali kwa kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri.

Korea Kusini haitambui haki ya kukataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri na wala haina mpango wa utumishi wa badala wa kiraia. Hivyo, Shahidi kijana anayekataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri anahukumiwa kifungo cha miezi 18 jela. Mashahidi vijana 40 hadi 50 wanafungwa kila mwezi. Baada ya kuachiliwa kutoka gerezani, vijana hao wanaendelea kuteseka kwa sababu wanawekwa kwenye rekodi ya wahalifu na wanahesabiwa kuwa wametoroka utumishi wa jeshi. Mashahidi wanakabili vizuizi vya kupata kazi na wanakosa mambo fulani katika jamii.

Wanaume ambao walipata mafunzo ya jeshi lakini sasa wamejifunza kuwapenda jirani zao na kutojifunza vita tena wanapata matatizo mbalimbali. Wanapokataa kwenda kupata mazoezi ya kijeshi kama wanajeshi wa akiba, wanaume hao huteswa na kutozwa faini.

Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limefanya maamuzi 500 kuhusu ukiukwaji wa haki za wanaokataa kujiunga na jeshi kwa sababu ya dhamiri nchini Korea Kusini na linaona vifungo vyao kuwa “vifungo visivyo na msingi wa kisheria.” Inadaiwa kwamba nchi ya Korea Kusini “ina daraka la kumaliza ukiukwaji huo wa haki” wakati ujao. Azimio la suala hili litamaanisha kwamba serikali ya Korea Kusini itaheshimu uhuru wa dini na dhamiri.