Hamia kwenye habari

Ndugu na dada pamoja na mawakili Mashahidi mbele ya Mahakama ya Utawala katika mji mkuu wa Mongolia, Ulaanbaatar.

AGOSTI 24, 2018
MONGOLIA

Ushindi wa Uhuru wa Kidini Nchini Mongolia: Mashahidi wa Yehova Wasajiliwa Tena

Ushindi wa Uhuru wa Kidini Nchini Mongolia: Mashahidi wa Yehova Wasajiliwa Tena

Mashahidi wa Yehova huko Ulaanbaatar, mji mkuu wa Mongolia, walipata cheti kutoka kwenye ofisi ya Baraza la Jiji Juni 14, 2018, kilichowapa ruhusa ya kusajili shirika lao la kidini.

Cheti cha kusajiliwa upya kinachowaruhusu Mashahidi wa Yehova wafanye mambo kisheria Ulaanbaatar.

Mashirika ya kidini nchini Mongolia yanahitaji kusajiliwa upya kila mwaka, na ndugu zetu walifanya hivyo bila matatizo tangu mwaka wa 1999 waliposajiliwa mara ya kwanza. Hata hivyo, mwaka wa 2015, Baraza la Jiji lilikataa kusajili upya shirika letu la kisheria huko Ulaanbaatar. Kisha, Januari 2017, Baraza la Jiji lilitoa uamuzi rasmi uliolikataza shirika hilo la kisheria kufanya shughuli zake za kidini. Wawakilishi wa Baraza walikataa kutoa uthibitisho waliotumia kutegemeza uamuzi wao. Ndugu waliamua kupinga uamuzi wa Baraza hilo kisheria.

Kesi ilipokuwa ikiendelea katika Mahakama ya Utawala, wakili wa Baraza la Jiji alijaribu kutoa uthibitisho akitumia uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu ya Urusi wa kufunga mashirika yetu ya kisheria nchini Urusi. Mawakili wetu wakasema kwamba uamuzi huo umechambuliwa na watu wa nchi nyingine na bado uko katika mahakama za kimataifa. Pia, mahakama ilikumbushwa kwamba uamuzi wa Urusi ulitolewa baada ya uamuzi wa Baraza la Jiji na hivyo hauwezi kutumiwa kutetea uamuzi wao.

Mahakama ya Utawala ilitangua uamuzi wa Baraza la Jiji na kukata kauli kwamba baraza hilo lilikuwa limefanya uamuzi bila kupata habari kamili na lilishindwa kuonyesha uthibitisho wa utendaji wowote usiofaa. Pia ilisema kwamba Baraza la Jiji lilikuwa limekiuka haki za msingi za ndugu hao, kutia ndani haki ya kutangaza imani ya kidini.

Jason Wise, mmoja wa mawakili wa Mashahidi katika kesi hiyo, alisema hivi: “Ingawa haki za msingi na uhuru hazitegemei kusajiliwa na Serikali, mara nyingi si rahisi kuabudu kwa uhuru bila kusajiliwa. Kati ya mambo mengine, shirika letu la kisheria linatusaidia kuingiza Biblia na machapisho ya Biblia kutoka nchi nyingine, kumiliki maeneo ya ibada, na kukodi maeneo ya makusanyiko. Tunafurahi kwamba Mahakama ya Utawala imetangua uamuzi wa Baraza la Jiji katika Ulaanbaatar na kutambua kwamba maamuzi kama hayo yanaathiri isivyofaa uhuru wetu wa ibada na kukusanyika nchini Mongolia.”