Hamia kwenye habari

Wahudhuriaji wa Kusanyiko la Eneo la 2023 la “Iweni na Subira”! Kushoto ni kusanyiko lililofanyika katika Kikrioli cha Jamaika mjini Old Harbour pamoja na picha ndogo ya programu katika lugha hiyo, na kulia ni kusanyiko lililofanyika katika Kijerumani cha Pennsylvania jijini Pittsburgh, Pennsylvania, Marekani pamoja na picha ndogo ya programu katika lugha hiyo.

OKTOBA 18, 2023
HABARI ZA ULIMWENGUNI POTE

Kwa Mara ya Kwanza Makusanyiko ya Eneo Yamefanyika Katika Kikrioli cha Jamaika na Kijerumani cha Pennsylvania

Kwa Mara ya Kwanza Makusanyiko ya Eneo Yamefanyika Katika Kikrioli cha Jamaika na Kijerumani cha Pennsylvania

Katika mwezi wa Julai 2023, kulikuwa na makusanyiko mawili ya eneo yaliyofanyika kwa mara ya kwanza uso kwa uso katika Kikrioli cha Jamaika na katika Kijerumani cha Pennsylvania. Kwa ujumla, karibu watu 2,000 walikusanyika pamoja kwa ajili ya kusanyiko walilokuwa wakitazamia kwa hamu la “Iweni na Subira”! lililofanywa katika lugha zao za asili.

Kikrioli cha Jamaika

Akina dada katika kusanyiko la Kikrioli cha Jamaika wakiwa wamesimama na bango linalosema, “Karibuni!”

Lugha kuu inayozungumzwa nchini Jamaika ni Kiingereza. Hata hivyo, watu wengi wanaoishi katika visiwa vya nchi hiyo wanazungumza pia Kikrioli cha Jamaika. Watu 1,700 hivi waliohudhuria kusanyiko hilo walikuja kutoka Uingereza na Marekani. Programu hiyo ilifanyika Julai 14 hadi 16, 2023 kwenye uwanja wa Marlie Technology ulio katika mji wa Old Harbour, nchini Jamaika. Watu kumi na wawili walibatizwa.

Ndugu na dada zetu wanaozungumza Kikrioli cha Jamaika walifurahi sana kusikiliza kusanyiko hilo kwa mara ya kwanza katika lugha yao ya asili. Dada Tenesha Gordon anasema hivi: “Niliposikia ndugu aliye jukwaani akitusalimia katika Kikrioli cha Jamaika mwanzoni mwa programu, machozi yalinilenga. Sikuamini kile nilichokuwa nikisikia. Sikutaka kusanyiko hilo liishe!”

Kijerumani cha Pennsylvania, Marekani

Wahudhuriaji wa kusanyiko wakiwa wamebeba bango linalosema, “Karibuni Kwenye Kusanyiko Letu la Eneo la Kwanza Katika Kijerumani cha Pennsylvania”

Karibu watu 400,000 hivi nchini Kanada na nchini Marekani wanazungumza Kijerumani cha Pennsylvania. Lahaja hiyo ya Kijerumani inazungumzwa na watu wanaoishi katika maeneo ya vijijini wanaoitwa Waamishi na Wamenno. Ndugu na dada walio katika makutaniko matano na kikundi kimoja cha Kijerumani cha Pennsylvania walisafiri kutoka katika majimbo mbalimbali ili kuhudhuria kusanyiko hilo lililofanyika Julai 7 hadi 9, 2023. Zaidi ya watu 200 walihudhuria programu hiyo katika Jumba la Kusanyiko la Coraopolis lililo Pittsburgh, Pennsylvania, Marekani.

Ndugu David Miller anatoka katika familia iliyozungumza Kijerumani cha Pennsylvania. Alianza kujifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova kwa Kiingereza zaidi ya miaka 25 iliyopita. Wakati huo, hakufikiri kungekuwa na makutaniko ya lugha yake, lakini sasa hata kuna kusanyiko katika lugha yake. Anasema hivi: “Nilifurahi sana! Nilikuwa makini sana kusikiliza programu hiyo kwa sababu ilifanyika katika lugha yangu. Mafundisho hayo yaligusa kabisa moyo wangu.”

Tunashangilia pamoja na ndugu na dada zetu ambao walihudhuria kusanyiko hili la kihistoria. Tunamshukuru sana Yehova anayetuunganisha na anayetoa nafasi kwa kila mmoja ya kupata lugha safi.​—Sefania 3:9.