Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Kishikizo cha Samaki Anayeitwa Remora

Kishikizo cha Samaki Anayeitwa Remora

 Samaki anayeitwa remora ana uwezo wa kujishikiza kwenye miili ya viumbe wengine wa baharini kwa nguvu sana, kisha yeye huachilia kwa wepesi bila kumdhuru kiumbe aliyembeba. Uwezo huo umewashangaza watafiti.

 Fikiria hili: Samaki huyo, remora, hujishikiza kwenye viumbe kama vile taa, papa, kasa, nyangumi, na viumbe wengine wa baharini bila kujali wana ngozi au magamba ya aina gani. Remora hula vimelea na mabaki ya chakula ya kiumbe aliyembeba. Wakati uleule remora husafirishwa na kulindwa na kiumbe huyo. Watafiti wanachunguza vishikizo vya remora, ili kuona jinsi samaki huyo anavyoweza kujishikiza kwa wororo lakini kwa nguvu juu ya maeneo mbalimbali.

 Samaki aina ya remora wakiwa wamejishikiza kwenye papa-nyangumi

 Kishikizo cha remora kilicho na umbo la yai kipo upande wa nyuma wa kichwa chake. Miisho ya kishikizo hicho ina unyama fulani mzito unaomwezesha kufyonza kwa nguvu. Ndani ya sehemu hiyo kuna aina fulani ya mifupa midogo. Pindo zake zinapojinyoosha, mifupa hiyo hugusa ngozi ya kiumbe aliyembeba na hivyo kutokeza msuguano. Mbinu hizo mbili za kufyonza na kutokeza msuguano humwezesha remora kujishikiza kwa nguvu hata ikiwa kiumbe aliyembeba atasonga kwa kasi au kubadili ghafla upande anaoelekea.

 Kwa sababu ya kustaajabishwa na kishikizo cha remora, wanasayansi wamebuni kishikizo kama hicho. Kifaa hicho kilicho na umbo la yai kinaweza kujishikiza kwenye sehemu mbalimbali. Wachunguzi hao walipofanya majaribio ya kung’oa kifaa hicho kwa kutumia uzito unaokizidi kwa mara mia moja, hawakufaulu!

 Teknolojia inayotegemea kishikizo cha remora inaweza kutumiwa kwa njia mbalimbali. Njia hizo zinatia ndani kuweka alama kwenye ngozi za viumbe wa baharini ili kuwafanyia uchunguzi, na pia kufanya uchunguzi katika maeneo ya bahari yenye kina kirefu. Vilevile inaweza kutumiwa kushikiza taa au vifaa vingine kwenye sehemu zilizo chini ya maji kwenye madaraja na meli.

 Una maoni gani? Je, kishikizo cha samaki anayeitwa remora kilijitokeza chenyewe? Au kilibuniwa?