Hamia kwenye habari

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Ngozi ya Mbilimbibahari

Ngozi ya Mbilimbibahari

 Mbilimbibahari ni wanyama wanaoishi kwenye sakafu ya bahari na kwenye matumbawe. Ngozi yao inaweza kuwa yenye matuta-matuta, au yenye miiba. Wana uwezo mkubwa wa kunyumbulika, kuwa laini kama nta au kubadilika na kuwa wagumu kama ubao ndani ya dakika au sekunde chache. Uwezo huo wa kunyumbulika huwasaidia mbilimbibahari kupenya kwenye mianya midogo na kuwa wagumu ili wasivutwe na kuliwa na wanyama wanaowinda. Siri ya mbilimbibahari ni ngozi yake yenye kustaajabisha.

 Fikiria: Ngozi ya mbilimbibahari inaweza kuwa katika hali tatu—ngumu, kawaida, na laini. Ili kubadili hali, mbilimbibahari hufunga au kufungua nyuzinyuzi zilizo kwenye ngozi zao. Wao hufanya hivyo kwa kutokeza protini mbalimbali zinazofanya ngozi iwe ngumu au laini.

 Protini zinazotokeza ugumu huunda madaraja madogomadogo, au minyororo, kati ya nyuzinyuzi kwenye tishu zinazounganisha, na kufanya ngozi iwe ngumu. Protini za kulainisha hufungua nyuzinyuzi hizo, na kufanya ngozi iwe laini. Ngozi ya mbilimbibahari inaweza kuwa laini sana kana kwamba inayeyuka.

 Wanayasansi wanatengeneza vifaa vyenye uwezo wa kubadilika kama ngozi ya mbilimbibahari. Mojawapo ya lengo lao ni kutokeza elektrodi zitakazotumiwa kwenye upasuaji wa ubongo zenye uwezo wa kuwa ngumu ili zifike kwenye sehemu hususa kisha ziwe laini. Uwezo huo wa kubadilika wa elektrodi utapunguza uwezekano wa kukataliwa na mwili.

 Una maoni gani? Je, ngozi ya mbilimbibahari ilitokana na mageuzi? Au iliumbwa?