Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Italia ilikuwa na maonyesho ya kwanza kwa ajili ya waliotalikiana. Waliohudhuria walitembelea mashirika ya ndoa ili kupata wenzi wapya, mashirika ya huduma za usafiri ili kupanga likizo kwa ajili ya waseja, na mashirika ya kupanga talaka ili kupata mawakili, wahasibu, wanasaikolojia, na wapatanishi wa familia.—CORRIERE DELLA SERA, ITALIA.

Kanisa Katoliki limeacha kuaminika kwa sababu “halijashughulikia vizuri kashfa za makasisi wanaowatendea watu vibaya kingono” na hilo “limetokeza tatizo kubwa sana katika usimamizi wa kanisa, huenda tangu lilipoanzishwa.”—NATIONAL CATHOLIC REPORTER, MAREKANI.

Wanasayansi waliochunguza chembe za urithi kutoka kwa nywele za mtu kutoka Greenland aliyekufa miaka 4,000 hivi iliyopita waligundua kwamba “inaonekana alikuwa mwenyeji wa Siberia.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, MAREKANI.

Watu Hawatumaini Sana Kanisa

“Watu wengi hawatumaini tena Kanisa [Katoliki],” kinasema kichwa kimoja kikuu katika gazeti The Irish Times. Ripoti hiyo inaorodhesha Kanisa Katoliki katika kikundi kimoja na mashirika mengine ambayo watu wengi nchini Ireland wameacha kuyaamini, kama vile, serikali na benki. Katika nchi inayojulikana sana kwamba watu ni washikamanifu kwa kanisa, zaidi ya nusu ya watu waliohojiwa katika uchunguzi wa hivi karibuni walisema kwamba ama hawalitumaini kanisa “kabisa” (asilimia 32) ama hawalitumaini kanisa “kwa kiasi kikubwa” (asilimia 21). Kashfa ambazo zimekumba kanisa hilo hivi karibuni zinasemekana kuwa ndizo zimewafanya watu wengi ‘wasilitumaini sana.’

Wahitimu wa Vyuo Hawana Kazi

Je, kupata elimu katika chuo kunakuhakikishia kwamba utapata kazi? Si kwa watu wengi, linasema gazeti Manila Bulletin. Gazeti hilo linamnukuu Herbert Bautista, meya katika jiji la Quezon City, akisema hivi: “Kila mwaka vyuo na vyuo vikuu vinatokeza mamilioni ya wahitimu ambao hukosa kazi kwa kuwa mafunzo yao hayapatani na kazi zilizopo.” Mwishowe, wengi huwa makarani au wanafanya kazi katika mikahawa. Serikali inawatia moyo wanaohitimu shule za sekondari wapate mafunzo mafupi yatakayowapa stadi za kazi au mambo ya kiufundi na hivyo kupata kazi kwa urahisi.

Daraja Linapata Kutu Kutokana na Mate

Huko Calcutta, India, Daraja la Howrah lenye urefu wa mita 457 linaathiriwa na mate ya wapita-njia. Kwa nini? Kwa sababu gutkha—mchanganyiko wa majani ya tambuu, kokwa la mpopoo, na limau iliyochachishwa na kufanywa kuwa ungaunga ambao hutafunwa na watu wengi kisha wanautema—ni mchanganyiko unaotokeza kutu upesi sana. Kulingana na gazeti la Calcutta The Telegraph, “tangu mwaka wa 2007, mate yote ya wapita-njia yamepunguza upana wa chuma kinacholinda nguzo [za daraja hilo] kutoka milimita sita hadi milimita tatu.” Wapita-njia 500,000 na magari 100,000 hupita kwenye daraja hilo kila siku.