Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Viumbe wa Ajabu Katika Pori la Tasmania

Viumbe wa Ajabu Katika Pori la Tasmania

Viumbe wa Ajabu Katika Pori la Tasmania

WAKATI wa mchana, kimya na utulivu hutanda katika pori la Tasmania. Lakini usiku, mingurumo na kelele zenye kuogopesha husikika msituni. Kelele hizo hutoka wapi? Zinatokezwa na mnyama aliye na mbeleko na jina lenye kushangaza​—ibilisi wa Tasmania (Tasmanian devil). Wanyama hao wenye nguvu wana sura yenye kuogopesha na sauti yenye kutisha, hasa wanapokula mzoga. Lakini kwa kweli wao si wanyama wenye kutisha.

Wanyama hao wanaweza kumaliza mizoga katika msitu upesi sana. Taya na meno yao yenye nguvu yanaweza kutafuna kila sehemu ya mzoga​—ngozi, mifupa, na kila kitu. Kwa kweli, mnyama huyo anaweza kula chakula kinacholingana na asilimia 40 ya uzito wa mwili wake katika muda wa dakika 30, na hiyo ni sawa na mwanadamu kula nyama yenye uzito wa kilo 25 mara moja!

Mnyama anayevutia zaidi ni wombati wa kawaida, mnyama mnene, mtulivu, na anayependeza. Wombati wa kike wana mbeleko nao hunyonyesha watoto wao. Lakini tofauti na mbeleko za wanyama wengine, mdomo wa mbeleko za wombati unaangalia nyuma, na hilo husaidia kuhakikisha kwamba mtoto hachafuki mama anapochimba shimo. Pia wana meno ambayo hayaachi kukua, na hilo huwasaidia sana kwa kuwa wao hutumia meno yao kuondoa vizuizi chini ya ardhi. Ingawa wanaonekana kuwa hawawezi kufanya mengi kwa sababu ya unene wao, wombati hao wana ustadi wa hali ya juu na wanaweza kubeba majani kwa kutumia miguu yao ya mbele na kuyaingiza mdomoni.

Mnyama mwingine mwenye kushangaza ni kinyamadege. Mnyama huyo anayeonekana kuwa wa ajabu-ajabu ana mdomo mrefu na miguu iliyo na utando kama ya bata, mwili na manyoya yake ni kama ya fisi-maji, na mkia kama wa buku. Pia yeye hutaga mayai kama kuku, anachimba mashimo ya chini ya ardhi kama wombati, na kunyonyesha kama dubu-jike. Si ajabu kwamba mwanasayansi wa kwanza kumchunguza alifikiri kuwa ni mnyama bandia!

Kwa nini tunafurahi kuwaona wanyama wa ajabu kama hao? Bila shaka ni kwa sababu Muumba wetu anataka tufurahie kuwaona. Biblia inaonyesha kwamba aliwaambia wanadamu wawili wa kwanza ‘watawale kila kiumbe hai juu ya dunia.’ (Mwanzo 1:28) Tunapowatazama wanyama kama hao katika mazingira yao ya asili, je, hilo halichochei tamaa yetu ya kutimiza mgawo huo?

[Picha katika ukurasa wa 11]

KUTEMBEA CHINI YA MAJITU

Ni vitu vichache vilivyo hai vinavyoweza kulinganishwa na ukubwa wa miti ya Tasmania. Mti mrefu zaidi ni mkalitusi wa aina fulani unaoitwa mountain ash (Eucalyptus regnans), ambao hukua kufikia mita 75 na pia huchanua maua. Mti mrefu zaidi katika eneo hilo una urefu wa mita 99.6, na hiyo ni mita 16 tu chini ya mti mrefu zaidi ulimwenguni, mti wa redwood unaopatikana huko California, Marekani.

Mti mwingine wa porini, msonobari unaoitwa Huon, unakaribia nusu ya urefu wa mti wa mountain ash, lakini unaweza kuishi mara sita zaidi ya mti huo. Wanasayansi fulani wanakadiria kwamba misonobari ya Huon inaweza kuishi kwa zaidi ya miaka 3,000, na basi ni mojawapo ya miti inayoishi muda mrefu zaidi duniani. Mti huo unaoitwa “mkuu” wa mbao za Tasmania huonwa kuwa mti wa pekee sana na watengenezaji wa vifaa vya mbao na mashua. Mbao zake za rangi ya manjano ni rahisi kutumia katika ujenzi na zina mafuta ya pekee ambayo huzihifadhi na kuwafukuza wadudu. Magogo yanayopatikana msituni ambayo yalianguka mamia ya miaka iliyopita bado yanaweza kutumiwa katika ujenzi.

[Picha katika ukurasa wa 10]

Ibilisi wa Tasmania

[Hisani]

© J & C Sohns/​age fotostock

[Picha katika ukurasa wa 11]

Wombati wa kawaida

[Picha katika ukurasa wa 11]

Kinyamadege

[Picha Hisani katika ukurasa wa 11]

Wombat and platypus: Tourism Tasmania; giant tree: Tourism Tasmania and George Apostolidis