Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

HABARI KUU | UHAI ULIANZAJE?

Maswali Mawili Muhimu

Maswali Mawili Muhimu

1 Uhai Ulianzaje?

BAADHI YA WATU WANASEMA NINI? Uhai ulitokana na vitu visivyo hai.

KWA NINI WENGINE HAWARIDHISHWI NA JIBU HILO? Leo, wanasayansi wanajua mengi zaidi kuhusu kemia na muundo wa chembe za viumbe kuliko zamani, lakini hawajafaulu kueleza uhai ni nini. Kuna tofauti kubwa sana kati ya chembe iliyo hai na vitu visivyo hai.

Wanasayansi wanakisia tu jinsi hali zilivyokuwa duniani mabilioni ya miaka iliyopita. Isitoshe, wana maoni yanayotofautiana kuhusu chanzo cha uhai. Kwa mfano, wengine wanasema kwamba uhai ulitokana na mlipuko mkubwa wa volkano na wengine wanasema ulitoka chini ya sakafu ya bahari. Pia wengine wanaamini kwamba molekuli za kwanza za uhai zilijitokeza katika anga za mbali na zikafika duniani zikiwa kwenye vimondo. Hata hivyo, maelezo hayo ya kisayansi hayatusaidii kuelewa jinsi uhai ulivyoanza.

Wanasayansi wanakisia pia kuhusu kuwepo kwa molekuli ambazo zilibadilika na kuwa chembe za urithi tunazojua leo. Inasemekana kwamba molekuli hizo zilitokana na vitu visivyo na uhai na hutokeza molekuli nyingine zinazofanana nazo. Hata hivyo, wanasayansi hawajathibitisha kwamba molekuli kama hizo zimewahi kuwepo na wala hawajafaulu kutengeneza hata moja kwenye maabara.

Viumbe hai vina uwezo wa pekee wa kuhifadhi na kuchanganua habari. Chembe hupeleka, huchanganua, na hutekeleza maagizo yanayohusu urithi yaliyo ndani yake. Baadhi ya wanasayansi hulinganisha habari zilizo kwenye chembe ya urithi na mfumo wa programu zilizo ndani ya kompyuta, ilhali muundo wa chembe hulinganishwa na kompyuta yenyewe. Hata hivyo, wale wanaotetea fundisho la mageuzi hawawezi kueleza chanzo cha habari zilizo ndani ya chembe ya urithi.

Molekuli za protini zinahitajika ili chembe ifanye kazi. Molekuli ya protini huwa na mamia ya amino-asidi ambazo zina mpangilio maalumu. Kwa kuongezea, molekuli hiyo ya protini lazima iwe na umbo fulani hususa ili itumike. Wanasayansi wengine wanasema kwamba haiwezekani chembe hata moja ya protini kujitokeza tu. Mtaalamu wa fizikia Paul Davies aliandika hivi: “Kwa kuwa chembe moja inahitaji maelfu ya protini mbalimbali ili ifanye kazi, basi haiwezekani kwamba zilijitokeza zenyewe.”

HITIMISHO. Baada ya utafiti wa kisayansi wa miaka mingi imebainika kuwa uhai unaweza kutokezwa tu na uhai mwingine.

Viumbe Hai Vilitoka Wapi?

BAADHI YA WATU HUSEMA NINI? Kiumbe cha kwanza kilikua hatua kwa hatua na kikabadilika na kutokeza viumbe mbalimbali, kutia ndani wanadamu, kupitia mabadiliko ya ghafla ya chembe za urithi na uteuzi wa asili.

KWA NINI WENGINE HAWARIDHISHWI NA JIBU HILO? Chembe hutofautiana. Kulingana na kitabu kimoja, inasemekana kwamba kueleza jinsi chembe ambazo si tata zilivyobadilika na kuwa tata ni fumbo gumu kwa wanamageuzi, kama ilivyo vigumu kwao kueleza chanzo cha uhai.

Wanasayansi wamegundua kwamba katika kila chembe, molekuli fulani za kipekee hushirikiana na molekuli za protini ili kufanya kazi mbalimbali. Kazi hizo zinatia ndani kusafirisha chakula, kubadili chakula kiwe nishati, kupeleka ujumbe, na kurekebisha sehemu mbalimbali za chembe. Je, mabadiliko ya ghafla ya chembe za urithi na uteuzi wa asili, ungeweza kutokeza chembe zinazofanya kazi kwa njia ya pekee kama hiyo? Watu wengi wanaona hilo haliwezekani.

Uhai wa wanadamu na wanyama huanza chembe mbili zinapounganika, ya kiume na ya kike. Baada ya muda chembe hizo huongezeka, hugawanyika, na hujipanga na kutokeza viungo mbalimbali vya mwili wa kiumbe kipya. Watu wanaoamini mageuzi hawawezi kueleza jinsi kila chembe inavyojipanga mahali pake.

Wanasayansi wametambua kwamba ili mnyama wa aina fulani abadilike na kuwa mnyama wa aina nyingine, mabadiliko hayo lazima yaanzie kwenye chembe. Kwa kuwa wanasayansi hawajathibitisha kwamba mageuzi yanaweza kutokeza hata chembe moja, basi ni wazi kwamba viumbe havikutokana na mabadiliko ya ghafla ya chembe za urithi wala uteuzi wa asili. Akizungumzia kuhusu maumbile ya wanyama, profesa wa biolojia Michael Behe anasema hivi: “Utafiti umeonyesha kwamba kuna viumbe wa aina nyingi, lakini utafiti huo haujathibitisha kwamba viumbe hao walitokana na vitu visivyo hai.”

Wanadamu wanajitambua, wanaelewa mazingira yao, na pia wana uwezo wa kufikiri na kujadiliana. Vilevile, wanaweza kuwa na maadili mazuri kama vile ukarimu, kujitoa, na haki. Sifa hizo nzuri za wanadamu haziwezi kusababishwa na mabadiliko ya ghafla ya chembe za urithi au uteuzi wa asili.

HITIMISHO. Ingawa watu wengi wanasisitiza kwamba uhai ulitokana na mageuzi, wengine hawajaridhishwa na nadharia hiyo na majibu inayotoa kuhusu chanzo cha uhai na kuenea kwa viumbe hai.