Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Piza Inapendwa Sana

Piza Inapendwa Sana

Piza Inapendwa Sana

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

INASEMEKANA kwamba Mfalme Ferdinand wa Kwanza (1751–1825) alivaa kama mtu wa kawaida na akatembelea eneo la watu maskini huko Naples. Kwa nini alifanya hivyo? Watu fulani wanasema kwamba alitaka kula chakula ambacho malkia alikataza kipikwe katika jumba la kifalme, yaani, piza.

Ikiwa Ferdinand angekuwa hai leo, angepata chakula hicho bila tatizo. Kwa sasa, kuna mikahawa 30,000 hivi ya kupikia piza nchini Italia, na kila mwaka mikahawa hiyo inapika piza za kutosha kila mtu nchini humo kupata 45!

Chanzo cha Piza

Huenda piza ilianza kupikwa huko Naples mnamo 1720. Wakati huo piza ilikuwa chakula cha maskini kilichopikwa haraka na kikauzwa na kuliwa nje. Wauzaji walitembea mitaani wakitangaza kwa sauti kubwa chakula chao kitamu. Piza hizo ziliwekwa kwenye chombo cha shaba kilichoitwa scudo, ambacho kilibebwa na wachuuzi kichwani.

Mwishowe Mfalme Ferdinand wa Kwanza aliwajulisha wasimamizi wa jumba la mfalme waziwazi kwamba alipenda piza. Muda si muda, chakula hicho kilichouzwa mitaani kilipendwa sana hivi kwamba matajiri na washiriki wa familia za kifalme walianza kuzuru mikahawa iliyouza piza. Mjukuu wa Ferdinand, Mfalme Ferdinand wa Pili hata aliamuru jiko la kuoka lililotumia kuni lijengwe katika mashamba ya Jumba la Kifalme la Capodimonte mnamo 1832. Kwa kufanya hivyo, alifaulu kuwafurahisha wageni wake wenye vyeo.

Je, Piza Ni Nzuri kwa Afya?

Leo, piza inapendwa sana na vijana, lakini tahadhari inahitajika. Ili piza iwe na lishe, inapaswa kupikwa kwa vyakula vyenye kiwango kinachofaa cha wanga, protini, na mafuta na ambavyo pia vina vitamini, madini, na asidi-amino nyingi. Inapendekezwa pia kwamba mafuta ya zeituni yatumiwe katika piza kwani yanachochea kutokezwa kwa HDL ambayo inaelezwa kuwa “aina nzuri ya mafuta inayosaidia kusafisha mishipa ya damu.”

Kwa kuongezea, piza inapopikwa vizuri ni mara chache inaposababisha tatizo la kumeng’enya. Sababu moja ni kwamba wanga ulio katika unga hupata kiasi kinachofaa cha maji wakati unapokandwa na kuchachishwa. Wakati huohuo, kuwepo kwa aina fulani ya wanga kunamfanya mtu ashibe haraka, jambo ambalo linasaidia hata mtu anayependa piza sana asile kupita kiasi.

Wakati utakapokula piza, kumbuka jinsi ilivyoanza. Na ufurahi kwamba Mfalme Ferdinand wa Kwanza hakuficha upendo wake wa piza.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27]

▪ Piza huiva vizuri inapopikwa katika jiko la kuoka linalotumia kuni. Moshi unaotokezwa wakati wa mapishi unafanya piza iwe na harufu tamu na majivu yanayobaki chini ya piza yanafanya iwe na ladha tamu.

▪ Katika mwaka wa 1990, piza kubwa zaidi ya mviringo ilitengenezwa. Ilikuwa na kipenyo wa mita 37, na ilikuwa na uzito wa tani zaidi ya 12!

▪ Mbinu ya zamani ya kurusha donge hewani na kulizungusha haifanywi bila sababu. Kwa kufanya hivyo donge hilo linatandazwa na miisho yake inainuka kidogo na kutokeza msingi mzuri wa piza!

[Picha katika ukurasa wa 26]