Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wataalamu wa Tiba wa Enzi za Kati

Wataalamu wa Tiba wa Enzi za Kati

MBINU nyingi za matibabu zinazotumiwa leo huenda si za kisasa kama wengine wanavyodhani. Kwa kweli, baadhi ya matibabu yanayotumiwa leo yalikuwepo karne nyingi zilizopita katika sehemu fulani za ulimwengu. Kwa mfano, chunguza historia ya tiba katika enzi za kati huko Mashariki ya Kati.

Katika mwaka wa 805 W.K., KHALIFA HARUN AR-RASHID alifungua hospitali katika mji wa Baghdad. Kuanzia karne ya 9 hadi ya 13, watawala wengine walijenga na kudumisha hospitali kotekote katika milki ya Kiislamu, kuanzia Hispania hadi India.

Hospitali hizo ziliwatibu matajiri na maskini wa dini zote. Mbali na kuwatibu watu, madaktari wenye uzoefu walifanya utafiti na kuwazoeza madaktari wapya. Kulikuwa na wadi tofauti kwa ajili ya matibabu tofauti-tofauti—matibabu ya watu wazima, matibabu ya macho, matibabu ya mifupa, upasuaji, magonjwa ya kuambukiza, na magonjwa ya akili. Madaktari, wakisaidiwa na wanafunzi wao, waliwachunguza wagonjwa kila asubuhi na kuwapa maelekezo kuhusu aina ya vyakula na madawa ya kutumia. Wataalamu wa madawa waliwapa wagonjwa dawa. Wasimamizi walihakikisha kwamba rekodi za wagonjwa zinatunzwa, walidhibiti matumizi ya fedha, walisimamia matayarisho ya chakula, na mambo mengine yanayohusiana na usimamizi​—kama tu ilivyo leo.

Wanahistoria wanaziona hospitali hizo za kale kuwa “mojawapo ya mafanikio makubwa ya jamii ya Kiislamu ya enzi za kati.” Katika eneo lote la milki ya Kiislamu, “maendeleo yaliyokuwa yakifanywa katika hospitali yangechangia pakubwa katika kusitawi kwa sayansi ya kitiba na matibabu kufikia wakati wetu,” anasema mwandishi na mwanahistoria Howard R. Turner.

RHAZES alizaliwa katikati ya karne ya tisa, katika jiji la kale la Rayy, ambalo sasa ni kitongoji katika jiji la Tehran. Anasemekana kuwa ndiye aliyekuwa “daktari bingwa katika eneo lote la Kiislamu na katika Enzi yote ya Kati.” Kwa ajili ya manufaa ya madaktari wengine, mwanasayansi huyo aliandika mbinu alizotumia kufanya majaribio mbalimbali, hali, vifaa alivyotumia, na matokeo aliyopata. Na aliwashauri madaktari wote kwenda sambamba na maendeleo ya kitiba katika vitengo vyao.

Rhazes alitimiza mambo mengi. Kwa mfano, maandishi yake ni sehemu ya kitabu chenye mabuku 23 kiitwacho Al-Hawi (Kitabu Chenye Habari Nyingi), ambacho ni miongoni mwa vitabu bora kabisa vya kitiba. Inasemekana kwamba kitabu hicho kinaeleza chanzo cha ukunga, elimu ya uzazi, na upasuaji wa macho. Kati ya maandishi yake 56 kuhusiana na habari za kitiba, kuna maandishi ya zamani zaidi yanayotegemeka kuhusu ugonjwa wa ndui na surua. Pia Rhazes aligundua kwamba homa ni moja ya njia ambazo mwili hujikinga.

Zaidi ya hayo, Rhazes alikuwa na hospitali katika miji ya Rayy na Baghdad, mahali ambako jitihada zake za kuwasaidia watu wenye matatizo ya akili zilifanya atambuliwe kuwa baba wa saikolojia na matibabu ya akili na ya kihisia. Mbali na habari za tiba, Rhazes alipata wakati wa kuandika vitabu kuhusu kemia, elimu ya nyota, hisabati, falsafa, na theolojia.

AVICENNA, mtaalamu mwingine katika nyanja ya kitiba alitoka Bukhara, eneo ambalo sasa ni sehemu ya Uzbekistan. Alikuwa miongoni mwa wataalamu wakuu wa kitiba, falsafa, elimu ya nyota, na hisabati wa karne ya 11. Avicenna aliandika ensaiklopedia inayoitwa The Canon of Medicine, ambayo ilizungumzia mambo yote yanayohusiana na elimu ya kitiba.

Avicenna aliandika katika kitabu hicho kwamba kifua kikuu ni ugonjwa wa kuambukiza, kwamba magonjwa yanaweza kuenezwa kupitia maji na udongo, kwamba hali ya kihisia huathiri afya ya mtu, na kwamba neva hupitisha habari kuhusu maumivu na ujumbe ili misuli ijibane. Kitabu hicho kinafafanua jinsi ya kutengeneza dawa 760 tofauti—kemikali zilizomo, utendaji wake, na pia magonjwa yanayotibiwa—na akaandika kanuni zinazopaswa kufuatwa wakati wa kufanyia majaribio dawa mpya. Kitabu hicho kilitafsiriwa katika Kilatini na kikaendelea kutumiwa kwa miaka mingi sana katika shule za kitiba huko Ulaya.

ALBUCASIS ni mtu mwingine anayejulikana sana katika historia ya tiba. Mvumbuzi huyo wa karne ya kumi, aliyeishi Andalusia, ambayo leo ni sehemu ya Hispania, aliandika muhtasari wenye mabuku 30, kutia ndani tasnifu yenye kurasa 300 kuhusu upasuaji. Katika tasnifu hiyo, alifafanua kuhusu mbinu za hali ya juu kama vile kumshona mtu aliyefanyiwa upasuaji kwa kutumia uzi ulitengenezwa kwa utumbo wa kondoo, kuondoa mawe kwenye kibofu kwa kutumia kifaa kinachopitishwa kwenye njia ya mkojo, upasuaji wa dundumio, na namna ya kuondoa mtoto wa jicho.

Albucasis alitumia mbinu ambazo zinafafanuliwa kuwa “za kisasa zaidi” ili kurahisisha matatizo yanayotokea wakati wa kujifungua na kurekebisha mabega yaliyoteguka. Alianza kutumia pamba ili kusafisha vidonda na akatumia plasta ili kuunga mifupa iliyovunjika. Pia alifafanua mbinu ya kurudisha meno yaliyotoka mahali pake, kutengeneza meno bandia, na kurekebisha meno yaliyoota vibaya, na kuondoa ukoga wa meno.

Kwa mara ya kwanza, michoro ya vifaa vya upasuaji ilipatikana katika tasnifu hiyo ya Albucasis. Ilikuwa na michoro 200 hivi ya vifaa vya upasuaji na miongozo ya jinsi ya kuvitumia na wakati wa kuvitumia. Ingawa miaka 1,000 imepita tangu wakati huo, baadhi ya vifaa hivyo havijabadilika sana.

Maarifa Yanaenea Mpaka Ulaya

Katika karne ya 11 na ya 12, wasomi hasa huko Toledo, Hispania, na pia huko Monte Cassino na Salerno, nchini Italia walianza kutafsiri vitabu vya kitiba vya Kiarabu katika Kilatini. Kisha madaktari walisoma vitabu hivyo katika vyuo vikuu vya maeneo yote ya Ulaya yaliyozungumza Kilatini. Ujuzi huo, wa kitiba wa Mashariki ya Kati “ulienea zaidi Ulaya katika karne zilizofuata, labda hata kuliko sayansi yoyote ya Kiislamu,” anasema mwandishi wa sayansi Ehsan Masood.

Ni wazi kwamba ugunduzi wa wataalamu wa Enzi za Kati kama vile, Rhazes, Avicenna, Albucasis, na wengine wengi walioishi katika kipindi hicho unaweza kusemwa kuwa msingi wa tiba ya kisasa.