Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 HABARI KUU

Ukweli Kuhusu Halloween

Ukweli Kuhusu Halloween

Je, Halloween, au Mkesha wa Sikukuu ya Watakatifu Wote husherehekewa unakoishi? Nchini Marekani na Kanada, Halloween ni maarufu sana na husherehekewa Oktoba 31, kila mwaka. Hata hivyo, desturi kama zile zinazofanywa wakati wa Halloween zimeenea katika sehemu nyingine nyingi ulimwenguni pote. Katika sehemu fulani, kuna sikukuu ambazo ingawa zimepewa majina tofauti, zina kusudi lilelile kama Halloween: kuwasiliana na viumbe wa roho iwe ni kupitia roho za wafu, wachawi, na hata ibilisi na malaika wake waovu.—Ona sanduku  “Sikukuu Zinazofanana na Halloween Ulimwenguni Pote.”

HUENDA wewe binafsi usiamini kwamba kuna viumbe wa roho wenye nguvu zisizo za kawaida. Huenda ukawa na maoni ya kwamba kushiriki katika sherehe ya Halloween na sherehe nyingine zinazofanana na hiyo ni njia ya kujifurahisha tu na ya kuwafundisha watoto wako kuwa wabunifu. Hata hivyo, watu wengi wanaona sikukuu hizo kuwa zenye madhara kwa sababu zifuatazo:

  1. Kitabu Encyclopedia of American Folklore (Ensaiklopedia ya Desturi za Wamarekani) kinasema: “Halloween inahusisha hasa kuwasiliana na viumbe wa roho, ambao wengi wao hutisha au kuogopesha.” (Ona sanduku  “Historia ya Halloween.”)  Vivyo hivyo, Halloween na sikukuu nyingine nyingi zina asili ya kipagani na huhusisha sana kuabudu mababu waliokufa. Hata leo, watu ulimwenguni pote hutumia siku hizo kuwasiliana na roho zinazosemekana kuwa za wafu.

  2. Ingawa Halloween huonwa kuwa sikukuu ya Wamarekani, kila mwaka idadi ya watu wanaoisherehekea katika nchi mbalimbali inazidi kuongezeka. Hata hivyo, watu wengi ambao wameanza kuisherehekea hivi karibuni hawajui kwamba ishara, mapambo, na desturi za Halloween, ambazo nyingi zinahusianishwa na viumbe wa roho wenye nguvu zisizo za kawaida na uchawi, zilitoka kwa wapagani.—Ona sanduku  “Chanzo Chake Ni Nini?”

  3. Maelfu ya wafuasi wa dini ya kiuchawi inayoitwa Wiccan, ambao hufuata desturi za Waselti wa kale bado huita Halloween kwa jina lake la kale, yaani, Samhain, nao husema kwamba huo ndio usiku mtakatifu zaidi katika mwaka. Likimnukuu mtu anayedai kuwa mchawi, gazeti USA Today lilisema hivi: “Wakristo ‘hawatambui kwamba wanasherehekea sikukuu yetu pamoja nasi. . . . Tunafurahia jambo hilo.’”

  4.   Sikukuu kama vile Halloween zinapingana na mafundisho ya Biblia. Biblia inaonya hivi: “Pasiwe mtu yeyote miongoni mwenu . . . apigaye ramli, wala mwaguzi, wala mpiga bao, wala mchawi, wala mlozi, wala mwenye kutaka kauli kwa mizimu na pepo au kutoka kwa wafu.”—Kumbukumbu la Torati 18:10, 11, Biblia Habari Njema; ona pia Mambo ya Walawi 19:31; Wagalatia 5:19-21.

Kwa sababu ya mambo yaliyozungumziwa katika makala hii, ni jambo la hekima kujua chanzo kisichofaa cha Halloween na sikukuu nyingine zinazofanana na hiyo. Kujua mambo kwa undani kutakusaidia kujiunga na wengine wengi ambao hawasherehekei sikukuu hizo.

“Wakristo ‘hawatambui kwamba wanasherehekea sikukuu yetu pamoja nasi. . . . Tunafurahia jambo hilo.’”—Gazeti USA Today, likimnukuu mtu anayedai kuwa mchawi

^ fu. 37 Neno la Kiingereza hallow ni neno la kale linalomaanisha “mtakatifu.” Siku ya Watakatifu Wote ni sikukuu ya kuwakumbuka watakatifu waliokufa. Katika Kiingereza Mkesha wa Siku ya Watakatifu Wote uliitwa All Hallow Even, baadaye ulifupishwa kuwa Halloween.