Hamia kwenye habari

Awamu ya 5 ya Picha za Uingereza (Septemba 2017 Hadi Februari 2018)

Awamu ya 5 ya Picha za Uingereza (Septemba 2017 Hadi Februari 2018)

Katika awamu hii ya picha, utaona jinsi ujenzi ulivyoendelea katika ofisi mpya ya tawi ya Mashahidi wa Yehova nchini Uingereza kati ya Septemba 2017 na Februari 2018.

Picha ya ofisi ya tawi ya Uingereza itakapokamilika jijini Chelmsford.

  1. Jengo la Studio ya Video

  2. Jengo la Udumishaji

  3. Jengo la Ofisi

  4. Makazi A

  5. Makazi B

  6. Makazi C

  7. Makazi D

  8. Makazi E

  9. Makazi F

Septemba 6, 2017​—Makazi C

Washiriki wa kikosi kinachoshughulikia upande wa nje wa majengo wakiunganisha matofali. Matofali hayo membamba yanaunganishwa kwa gundi ili kuficha nguzo za chuma zinashikilia kuta.

Septemba 20, 2017​—Makazi D

Mshiriki wa kikosi cha wachora-ramani anatia alama mahali ambapo kuta za nje za vyumba zitakuwa, akitumia kifaa cha kupima. Wakati huohuo, kazi ya useremala inaendelea kufanywa katika Makazi F, yanayoonekana upande wa nyuma.

Septemba 27, 2017​—Makazi F

Mtu akinyunyiza mvuke kwenye ukuta na kuulainisha kwa kifaa. Ili kuhifadhi maji, idara inayoshughulikia sehemu za kumalizia inateka maji kutoka katika kifaa kinachopunguza umajimaji chumbani na kuyatumia kuchanganya zege na niru kwa ajili ya kuweka vigae.

Oktoba 3, 2017​—Eneo la ujenzi wa ofisi ya tawi

Nje ya Makazi E, wakandarasi wakitengeneza barabara inayounganisha barabara kadhaa.

Oktoba 10, 2017​—Makazi F

Mjenzi wa kutumia matofali mwenye umri wa miaka 71 anajenga ukuta wa nje wa Makazi F. Tangu ujenzi huu uanze Mashahidi zaidi ya 100 wenye umri wa zaidi ya miaka 70 wamechangia ustadi na uzoefu wao wenye thamani.

Novemba 16, 2017​—Makazi

Picha ya angani kutoka upande wa magharibi. Majengo yote ya makazi yatakuwa na paa za pekee. Paa zitakapofunikwa, kuzuiwa zisiingize maji, na sehemu ya kuruhusu maji yapite inapotayarishwa, mbegu za mimea inayopatikana katika eneo hilo zinaweza kupandwa. Paa kama hizo zinanufaisha wanyama-pori, zinapunguza gharama za nishati, na zinasaidia kudhibiti maji ya mvua. Sehemu ya mbele kuna msingi wa Makazi A na msingi wa sehemu fulani ya jengo la ofisi.

Novemba 21, 2017​—Makazi F

Maseremala wanaweka fremu ya mlango iliyotayarishwa mapema kwenye mwingilio fulani wa jengo. Milango hiyo pamoja na fremu zake zinapofikishwa kwenye eneo la ujenzi hazihitaji kupakwa rangi bali zinakuwa tayari kutumiwa, na hivyo kuzifanya ziwe rahisi kuingiza.

Novemba 28, 2017​—Jengo la Ofisi

Jua linapoanza kutua, wakandarasi wanasimamisha misingi kwa ajili ya jengo la ofisi. Kwenye sehemu ya kati ya picha hiyo, wakandarasi wanaingiza chuma ndani ya mashimo yenye kina cha mita 20 hivi yaliyojazwa zege. Makazi B yanaonekana upande wa nyuma wa picha.

Desemba 5, 2017​—Makazi E

Mfanyakazi akining’iniza vitu vya kushikilia mabomba ya kupasha joto yaliyo kwenye dari sehemu ya kuegesha magari. Dari hiyo imewekewa mbao fulani zitakazopunguza baridi inayofika kwenye sakafu ya sehemu ya juu ya makazi.

Desemba 8, 2017​—Makazi F

Mshiriki wa kikosi cha kumalizia sehemu za nje anapiga msasa kuta ili kuzitayarisha kufunikwa. Mashimo madogo sana yanaruhusu vumbi lote kutolewa kupitia kifaa hicho.

Desemba 21, 2017​—Eneo la ujenzi wa ofisi ya tawi

Watu wawili wanatengeneza sehemu ya juu ya barabara. Wakitumia kifaa chenye moto, wanachoma na kusababisha matundu yatakayoruhusu nyasi kukua. Kufanya hivyo kunapunguza kasi ya maji ya mvua.

Desemba 26, 2017​—Makazi F

Wapaka-rangi wakipaka rangi mara ya mwisho sehemu fulani ya jikoni.

Desemba 28, 2017​—Makazi F

Watu wakifungua sehemu fulani za ngazi ili kutengeneza varanda. Mabomba mekundu yaliyo sehemu ya kati ya picha yanaingiza hewa yenye joto wakati wa majira ya baridi kali ili kukausha sakafu, kuta, na sehemu zilizopakwa rangi.

Januari 16, 2018​—Makazi F

Akitumia kifaa, mtu mmoja anaondoa hewa yoyote iliyojikusanya kwenye kuta zilizofunikwa. Hilo linafanya iwe rahisi kudumisha na kusafisha kuta hizo ambazo watu wengi wanapita. Sehemu ya nyuma washiriki wengine wa kikosi hiki wanapaka ukuta rangi na kukata kitu hicho cha kufunika kuta.

Januari 27, 2018​—Makazi E

Wafanyakazi wakihudhuria mkutano kabla ya kuanza kazi siku hiyo. Msimamizi wa kikundi hicho anazungumzia umuhimu wa kutanguliza usalama na mambo yanayoweza kuhatarisha usalama. Wafanyakazi wa idara mbalimbali walijitolea kufanya kazi muda wa ziada ili kusafisha Makazi F na eneo lililozunguka kabla ya watu wa kwanza kuhamia.

Februari 1, 2018​—Makazi F

Wakitumia lifti, wakandarasi wanamaliza kuweka varanda kwenye Makazi F. Rangi ya varanda hizo imekusudiwa kutambulisha majengo na inafanana na majani maridadi yanayochipuka hapo wakati wa majira ya kupukutika. Sehemu ya nyuma, kitu cha kuzuia jengo lisiathiriwe na mabadiliko ya hewa kinaondolewa kutoka Makazi E kabla ya ngazi kufunguliwa.

Februari 3, 2018​—Makazi

Wakati wao wa ziada, wenzi hawa wa ndoa wanahamishia vitu vyao kwenye Makazi-F yaliyokamilika siku moja kabla. Kwa kuwapa wafanyakazi wa ujenzi makao katika majengo hayo mapya, gharama za kodi na usafiri zinapungua na wafanyakazi wanaweza kufanya mengi zaidi.

Februari 12, 2018​—Makazi A

Wakandarasi wamwaga zege kwenye eneo la kuegesha magari wakati wa jioni. Makazi B yanaonekana upande wa nyuma.

Februari 15, 2018​—Makazi E

Mume na mke maseremala wakikata vigae vya jikoni, wakitumia msumeno unaofyonza vumbi. Kuvikata karibu na mahali vitakapowekwa kunapunguza hatari ya kuvivunja wakati wa kuvisafirisha.