Hamia kwenye habari

Akina ndugu wakiwa kando ya barabara wakisubiri usafiri wa kuwapeleka sehemu salama

JANUARI 2, 2024
SUDAN

Ndugu na Dada Walazimika Kukimbia Vita kwa Mara Nyingine Nchini Sudan

Ndugu na Dada Walazimika Kukimbia Vita kwa Mara Nyingine Nchini Sudan

Akina ndugu wakiwa wamembeba mwabudu mwenzao ambaye ni mgonjwa walipokuwa wakikimbia kutoka Wad Madani

Desemba 15, 2023, vita vinavyoendelea kati ya vikundi viwili vyenye silaha kwenye mji mkuu wa Sudan, Khartoum, vilienea hadi kufikia Wad Madani, jiji la pili kwa ukubwa nchini humo. Kama ilivyoripotiwa awali kwenye jw.org, vita hivyo vilipoanza jijini Khartoum mwezi Aprili 2023, ndugu na dada zetu wengi walikimbilia jiji la Wad Madani, lililo umbali wa kilomita 170 hivi kusini-mashariki kutoka Khartoum. Sasa zaidi ya ndugu na dada 150 kati ya hao wamelazimika kukimbia tena kutokana na vita vinavyoendelea.

Athari Ambazo Ndugu na Dada Zetu Wamepata

  • Hakuna ndugu au dada ambaye amejeruhiwa au kuuawa

  • Angalau ndugu na dada 158 hivi wamelazimika kuhama makao yao. Baadhi yao wamekimbilia kwenye majiji au nchi jirani

  • Ndugu na dada 10 pamoja na watu wao wa ukoo ambao si Mashahidi wamebaki Wad Madani

Jitihada za Kutoa Msaada

  • Waangalizi wa mzunguko na wazee wa eneo hilo wanaandaa msaada wa kiroho kwa wale walioathiriwa

  • Halmashauri za Kutoa Msaada nchini Sudan na katika nchi jirani zinashirikiana ili kuandaa na kutoa msaada unaotia ndani chakula, dawa, na malazi

Ndugu na dada zetu saba ambao walibatizwa kwenye kusanyiko huko Wad Madani siku chache kabla ya vita kuanza jijini humo

Jambo lenye kupendeza ni kwamba juma moja tu kabla ya vita kuanza jijini Wad Madani, ofisi ya tawi ya Afrika Mashariki ilifanya mipango kwamba waliokuwa wamekimbia watazame programu iliyorekodiwa ya Kusanyiko la Eneo la 2023 lenye kichwa “Iweni na Subira!” katika Kiarabu. Miongoni mwa watu 200 hivi waliotazama programu hiyo kulikuwa na ndugu na dada 145 ambao walikimbia kwa sababu ya vita vilivyotokea jijini Khartoum. Wengi kati ya wale waliohudhuria kusanyiko hilo walishukuru sana kupata chakula cha kiroho kwa wakati unaofaa. Waliohudhuria kusanyiko hilo walitiwa moyo hasa na drama inayotegemea Biblia yenye kichwa “Mkabidhi Yehova Njia Yako,” ambayo ilikazia hali zinazofanana na zile walizokabili. Kwa kuongezea, watu saba walibatizwa katika kusanyiko hilo.

Tunasali kwamba ndugu na dada zetu nchini Sudan waendelee kuvumilia hali hiyo ngumu, na tunatazamia kwa hamu wakati ambapo Yehova ‘atakomesha vita katika dunia yote.’​—Zaburi 46:9.