Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Hali ya Hewa Inavyoweza Kubadili Historia

Jinsi Hali ya Hewa Inavyoweza Kubadili Historia

Jinsi Hali ya Hewa Inavyoweza Kubadili Historia

HISTORIA iliyorekodiwa inaonyesha jinsi hali ya hewa ilivyoathiri matukio fulani muhimu. Hebu tuchunguze matukio mawili.

Dhoruba Ilipopiga

Mnamo 1588, Mfalme Philip wa Hispania alituma msafara wa meli, zilizojulikana kama Manowari za Hispania, kushambulia Uingereza. Lakini mambo yalimwendea mrama kwani hali ya hewa ilivuruga kabisa mipango yake.

Msafara wa meli hizo za Hispania uliingia kwenye Mlango-Bahari wa Uingereza na kukutana na meli za Uingereza. Meli hizo za Uingereza zinazoweza kuendeshwa kwa urahisi zilishambulia zile za Hispania lakini zikaharibu chache tu. Kisha, Manowari za Hispania zikatia nanga katika bandari ya Calais ili kuchukua wanajeshi wa kuvamia Uingereza.

Ilipokuwa usiku, majeshi ya Uingereza yaliwasha moto meli zake kadhaa, na kuziacha zielee zikisukumwa na upepo bila kuongozwa na mtu yeyote na kuelekea meli za Hispania zilizokuwa zimetia nanga. Wanajeshi wa meli za Hispania walikata nanga nyingi ili kukwepa meli hizo za Uingereza zilizokuwa zikiwaka moto. Hatua hiyo ya Wahispania iliwaletea matatizo baadaye.

Baada ya kisa hicho kilichotokea huko Calais, meli zote zilielekea kwenye Bahari ya Kaskazini, huku upepo ukizisukuma kutoka upande wa nyuma. Kufikia sasa, majeshi ya Uingereza yalikuwa yameishiwa na silaha, hivyo yakatia nanga kwenye pwani ya Uingereza. Kwa kuwa Waingereza walizuia Manowari za Hispania zisiweze kurudi Hispania na upepo ulikuwa ukipiga dhidi ya meli hizo, Wahispania walilazimika kusafiri kuelekea upande wa kaskazini kuzunguka Scotland, halafu waelekee kusini kupita Ireland, kisha warudi Hispania.

Kufikia wakati huu, meli za Hispania zilikuwa zimeishiwa kabisa maji na chakula, na zile zilizokuwa zimeharibiwa zilikuwa zikiwasafirisha wanajeshi wengi waliokuwa wamejeruhiwa vibaya pamoja na wengine waliokuwa wakiugua kiseyeye. Kwa hiyo, wasafiri wote walipimiwa sana chakula na hivyo wakazidi kuwa hoi.

Baada ya meli hizo kuzunguka Scotland, dhoruba kali sana kutoka Bahari ya Atlantiki ilipiga meli hizo na kuzisukuma kuelekea ufuo wa Ireland. Kwa kawaida, chini ya hali hizo wangetia nanga na kusubiri dhoruba hiyo ipite. Hata hivyo, kwa sababu nyingi ya nanga zilikuwa zimekatwa wakati wa mashambulizi ya hapo awali, meli 26 za Hispania zilivunjika kwenye pwani ya Ireland, na kusababisha vifo vya wanaume kati ya 5,000 na 6,000.

Kufikia wakati Manowari hizo ziliporudi Hispania, karibu watu 20,000 walikuwa wamekufa. Kwa kweli hali mbaya ya hewa ndiyo hasa iliyosababisha vifo vya watu hao wote na kuharibu meli hizo. Inaonekana kwamba Waholanzi waliamini hivyo. Baadaye, walipotengeneza medali ya kukumbuka kushindwa kwa Manowari za Hispania, walitangaza wazi imani iliyokuwa imeenea sana kwamba Mungu husababisha misiba ya asili na hivyo wakaandika hivi kwenye medali hiyo: “Yehova alipuliza nao wakatawanyika.”

Washindwa kwa Mvua

Tukio lingine lililobadili ulimwengu ambalo liliathiriwa sana na hali ya hewa ni Pigano la Waterloo la mwaka wa 1815. Historia inaonyesha kwamba katika vita hivyo vilivyopiganwa huko Waterloo, kilomita 21 kusini mwa Brussels, Ubelgiji, zaidi ya wanaume 70,000 waliuawa au kujeruhiwa kwa muda wa saa chache tu. Dyuki Mwingereza wa Wellington alichagua uwanja huo wa pigano na akachagua sehemu iliyokuwa imeinuka. Ingawa majeshi ya Ufaransa yaliyoongozwa na Napoleon yalikuwa mengi kuliko yale ya Wellington, Napoleon alihitaji kushinda maadui wake kabla ya giza kuingia, kwa sababu Wellington angepata askari zaidi wa kumsaidia kutoka kwa jeshi la Prussia usiku huo. Hata hivyo, kwa mara nyingine tena, hali ya hewa iliathiri sana mipango yake.

Mvua kubwa sana ilinyesha usiku uliotangulia vita hivyo. Wanajeshi wengi walikumbuka usiku huo kuwa usiku mgumu zaidi maishani mwao. Hata ingawa wengine wao walifaulu kusimamisha mahema madogo, mwanajeshi mmoja alisema kwamba vitanda vilivyokuwa ndani ya mahema hayo vilikuwa vimelowa kana kwamba vilikuwa ndani ya ziwa. Ardhi ililowa maji na kuwa kama kinamasi. Ili afaulu kushinda jeshi la Wellington, Napoleon alitaka kuanza mashambulizi yake alfajiri. Hata hivyo, hakufaulu kushambulia hadi baada ya saa kadhaa.

Sababu kuu iliyofanya achelewe kufanya mashambulizi hayo ni kwa sababu ardhi ilikuwa imelowa sana, ilihitajika ikauke kwa kiasi fulani ili vita vianze. Pia, matope yalizuia uwezo wa mizinga ambayo Napoleon alipendelea zaidi kutumia. Kwanza, ilikuwa vigumu kwao kusogeza vifaa hivyo kwenye matope na hilo likapunguza uwezo wao wa kurusha mizinga. Pili, matufe ya mizinga hiyo yalihitajika kugonga ardhi kisha yawalipukie wanajeshi wa Wellington kwa kadiri kubwa zaidi. Hata hivyo, yote hayo hayakuwezekana kwa sababu ardhi ilijaa matope, na hivyo mizinga haikuweza kulipuka kama ilivyokusudiwa. Hilo lilichangia sana kufanya Napoleon na majeshi yake washindwe. Hivyo, kwa sababu ya hali mbaya sana ya hewa, majeshi ya Napoleon yalishindwa, na akapelekwa uhamishoni.

Kutokana visa hivyo, ni wazi kwamba hali ya hewa iliathiri sana matukio muhimu ya ulimwengu. Mambo hayo yalichangia sana kuibuka kwa Milki ya Uingereza.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Manowari za Hispania

[Hisani]

© 19th era/Alamy

[Picha katika ukurasa wa 25]

Pigano la Waterloo

[Hisani]

© Bettmann/CORBIS